“Sasa hivi bila kuwa na video nzuri wimbo haufiki popote,” hii ni
kauli ambayo nimekuwa nikiisikia sana kutoka kwenye vinywa vya wasanii
wa Tanzania.
Kiukweli ni kauli yenye ukweli kwa mazingira yalivyo sasa. Na nadhani
ni kwasababu mapinduzi ya teknolojia yaliyofanya matumizi ya simu yawe
makubwa, yamewafanya mashabiki wengi wa muziki kuwa na uwezo wa muda
wote kuangalia video kwenye simu zao. Watu hawategemei tena kusubiri
kuona video za muziki kwenye TV tu.
Na ukweli ni kwamba siku hizi mashabiki wanapenda sana kuangalia
kuliko kusikiliza tu. Hali hiyo imewafanya wasanii kuumiza vichwa sana
kutengeneza video nzuri kwaajili ya ngoma zao.
Miaka ya nyuma, mambo hayakuwa hivyo. Video zilikuwa chache sana na
pengine ni kwasababu hakukuwepo na waongozaji wengi wa video. Pamoja na
hivyo, hits nyingi sana zilizaliwa. Kipindi hicho maproducer kama
P-Funk, Master J, Mika Mwamba, Roy na wengine walitengeneza ngoma
zilizosumbua mawimbi ya redio na kuingia kwenye vichwa vya watu bila
hata kuwa na video.
Hits kibao za wasanii kama Juma Nature, Profesa Jay, Jay Moe, Ngwair,
Mwana FA, AY na wengine hazikuwa na video lakini bado zilihit ile
mbaya. Katika kipindi hiki ambacho uhakika wa mtu kuipata ngoma ni
rahisi zaidi kuliko zamani, iweje tuamini kuwa wimbo hauwezi kufanya
vizuri kama hauna si video tu, bali video nzuri? Yaani imefika wakati
kama wimbo hauna video basi kuna nyota fulani zinatolewa au kwa lugha
nyingine wimbo unakuwa na kasoro.
Mimi bado naamini kuwa wimbo unaweza ukahit na kuwa anthem bila hata
ya kuwa na video na kutokana na kufanya kwake vizuri, kunakuwepo na
demand kubwa zaidi kutoka kwa mashabiki ya watu kutaka video yake.
Wakati mwingine nahisi nyimbo zinashindwa kufanya vizuri si kwasababu
hazina video bali ni za kawaida mno. Au wakati mwingine wasanii huumiza
zaidi kichwa na kutumia gharama kubwa kufanya video nzuri kwa nyimbo za
kawaida au mbaya. Yaani msanii anaingia studio kurekodi wimbo
akimfikiria zaidi director wa video atakavyoifanya video hiyo bila
kufikiria kwanza kutengeneza hit studio.
Na ndio maana wasanii wengi wapo radhi kumlipa producer shilingi
lakini tano na kwenda kufanya video ya shilingi milioni 30 South.
Wasanii hawaumizi tena kichwa kutengeneza nyimbo bora bali wanafikiria
tu kutengeneza video bora ili nao waonekane MTV Base au Trace TV.
Ndio maana kuna nyimbo kibao zina video nzuri lakini hata hazikiki
kitaa ni kwasababu ni mbovu. Na wengine wameishia kuwa na stress baada
ya kutumia fedha nyingi kufanya video za nyimbo ambazo hazifiki popote.
Ni sawa na kuupaka mafuta na manukato mwili wako bila kuoga.
Ngoma nyingi sana zinapigwa nusu nusu na hivyo kuhit yenyewe inakuwa
jambo gumu. Hata kama ikiwa na video ya $20,000, itapotea fasta kwenye
masikio.
Juzi nilikutana na Master J na nilimdadisi sana kuhusu utayarishaji
wa muziki uliochezwa live. Nilimuuliza inagharimu kiasi gani kuchukua
bendi kwa mfano Njenje au Inafrica na kumsaidia msanii kucheza vyombo na
kuurekodi wimbo live. Alisema gharama kubwa zaidi inaweza kuwa shilingi
milioni moja na gharama ndogo tu za kuwawezesha wapiga vyombo wakati wa
kufanya mazoezi.
Kwahiyo inawezekana kabisa kutengeneza wimbo mzuri na uliokamilika
kwa gharama ndogo na pindi unapoipa video nzuri, una uhakika wa kuwa na
wimbo utakaodumu kwa miaka mingi bila kuchosha masikio ya wapenzi wa
muziki. Ni kwasababu kamwe haitakuja kutokea muziki uliotengenezwa na
mtu mmoja kuwa sawa na ule uliotayarishwa na watu wengi na tena live.
Kwahiyo inawezekana kabisa kuwa na nyimbo zitakazofanya vizuri bila
hata kuwa na video. Video ni muhimu sana kwenye tasnia ya muziki lakini
wasanii waache kuweka nguvu nyingi huko na kusahau kutengeneza muziki
mzuri.
No comments:
Post a Comment